Date: 
16-06-2025
Reading: 
Isaya 48:9-16

Utatu Mtakatifu 

Jumatatu asubuhi tarehe 16.06.2025

Isaya 48:9-16

9 kwa ajili ya jina langu nitaahirisha hasira yangu, na kwa ajili yako nitajizuia, ili nisifiwe, wala nisikukatilie mbali.

10 Tazama, nimekusafisha, lakini si kama fedha; nimekuchagua katika tanuru ya mateso.

11 Kwa ajili ya nafsi yangu, kwa ajili ya nafsi yangu, nitatenda haya; je! Litiwe unajisi jina langu? Wala sitampa mwingine utukufu wangu.

12 Nisikilize mimi, Ee Yakobo; na Israeli, niliyekuita; mimi ndiye. Mimi ni wa kwanza, na mimi ni wa mwisho pia.

13 Naam, mkono wangu umeuweka msingi wa dunia, na mkono wangu wa kuume umezitanda mbingu; niziitapo husimama pamoja.

14 Kusanyikeni, ninyi nyote, mkasikie; ni nani miongoni mwao aliyehubiri haya? Bwana amempenda; atatimiza mapenzi yake juu ya Babeli, na mkono wake utakuwa juu ya Wakaldayo.

15 Mimi, naam, mimi, nimenena; naam, nimemwita; nimemleta, naye ataifanikisha njia yake.

16 Nikaribieni, sikieni haya; tokea mwanzo sikunena kwa siri; tangu yalipokuwapo, mimi nipo; na sasa Bwana MUNGU amenituma, na roho yake.

Mungu mmoja: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu;

Isaya alitumwa kuleta habari za Mungu muumbaji na Mwokozi wa wana wa Israeli waliokuwa uhamishoni. Mungu kupitia Isaya anawaambia kuahirisha hasira yake, anaahidi kuwasafisha na kuwaondoa kwenye mateso. Mungu anawaambia Israeli kwamba ndiye aliyewaita, yeye ndiye wa kwanza na wa mwisho. Bwana anaendelea kuwaita Israeli wakusanyike mbele zake kwa kumcha, maana ndiye Mungu muumbaji na Mwokozi wao.

Mungu anawaita Israeli kumrudia, akiahidi kuahirisha hasira yake. Hii ni ahadi ya Mungu kuwasamehe dhambi watu wake, kama ambavyo hutusamehe sisi hata sasa. Mungu ndiye mwanzo na mwisho, yaani yeye ndiye muumbaji na Mwokozi mwenye hatma yetu. Mungu alikuwa anawaahidi Israeli kuahirisha hasira yake kwa walivyokuwa uhamishoni, yaani kuwarudisha katika nchi yao. Hii ndiyo ahadi ya kutusamehe dhambi zetu pale tunapomwamini yeye muumbaji wetu aliyetuokoa kwa njia ya kifo cha Yesu msalabani, na kututakasa kwa Roho Mtakatifu. Tunakumbushwa kumcha yeye daima katika maisha yetu ili tuwe na mwisho mwema. Amina

Uwe na wiki njema

Heri Buberwa