Date: 
02-07-2025
Reading: 
Tito 1:1-4

Jumatano asubuhi tarehe 02.07.2025

Tito 1:1-4

1 Paulo, mtumwa wa Mungu, na mtume wa Yesu Kristo; kwa ajili ya imani ya wateule wa Mungu, na ujuzi wa kweli ile iletayo utauwa;

2 katika tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu asiyeweza kusema uongo aliuahidi tangu milele;

3 akalifunua neno lake kwa majira yake katika ule ujumbe niliowekewa amana mimi kwa amri ya Mwokozi wetu Mungu;

4 kwa Tito, mwanangu hasa katika imani tuishirikiyo. Neema na iwe kwako na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Mwokozi wetu.

Wito wa kuingia Ufalme wa Mungu;

Andiko la Paulo kwa Tito linaendana na lile la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Timotheo, kwa sehemu kubwa ikiwa ni mambo yanayotakiwa kwa viongozi wa Kanisa, maaskofu na wazee (sura 1) wanapokabiliwa na mafundisho ya uongo. Na sura ya 2 (2:1-10) namna ya kuwatendea watu wa makundi mbalimbali ya Jumuiya ya Kikristo. Paulo anamhimiza na kumtia moyo Tito kuwa imara na kulipa Kanisa mafundisho ya kiroho (sura ya 3)

Sasa somo la asubuhi hii ni salamu, ambayo ni utangulizi wa hayo yote. Paulo anamtakia Tito neema na amani zitokazo kwa Mungu, ili aweze kupeleka ujumbe wa Mungu kwa Kanisa lake kama anavyotumwa. Tito anatumwa kulifundisha Kanisa la Mungu mambo yapasayo waamini kutenda kama Paulo anavyomsalimia. Yaani Tito anatumwa kufanya kazi ya kuutangaza Ufalme wa Mungu, ambao nasi asubuhi hii tunakumbushwa kukaa katika Kristo ili asituache katika huo Ufalme wake. Amina

Siku njema

Heri Buberwa