Date:
04-08-2025
Reading:
1 Mambo ya nyakati 28:-19-20
Jumatatu asubuhi tarehe 04.08.2025
1 Mambo ya Nyakati 28:19-20
19 Hayo yote, akasema Daudi, yamenielea kwa maandiko kutoka kwa mkono wa Bwana, naam, kazi zote za mfano huu.
20 Kisha Daudi akamwambia Sulemani mwanawe, Uwe hodari, mwenye moyo mkuu, ukatende hivyo; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu, Mungu wangu, yu pamoja nawe; yeye hatakupungukia wala kukuacha, hata itakapomalizika kazi yote ya huo utumishi wa nyumba ya Bwana.
Tunaitwa kuzaa matunda mema;
Somo la asubuhi ya leo ni sehemu ya hotuba ya Daudi huko Yerusalemu. Alikusanya watu akaanza kuwahutubia, kwamba alitamani kuijenga nyumba ya Bwana, lakini Bwana alimwambia kuwa yeye (Daudi) asingeweza kuijenga nyumba ya Bwana, maana alikuwa mtu wa vita, alimwaga damu. Badala yake Daudi anahutubia akisema kuwa Bwana alimchagua Suleimani kuijenga nyumba yake. Angalia;
1 Mambo ya Nyakati 28:5-7
5 tena katika wana wangu wote (kwani Bwana amenipa wana wengi), amemchagua Sulemani mwanangu ili aketi juu ya kiti cha enzi cha ufalme wa Bwana, juu ya Israeli. 6 Akaniambia, Sulemani, mwanao, ndiye atakayeijenga nyumba yangu na nyua zangu; kwa kuwa nimemchagua awe mwanangu, nami nitakuwa babaye. 7 Na ufalme wake nitauweka imara milele, akijitia kwa bidii kuzitenda amri zangu na hukumu zangu, kama hivi leo.Ndipo Daudi katika hotuba yake anaendelea kumwambia Suleimani kwamba amechaguliwa kujenga nyumba ya Bwana. Mstari wa 19 unamtia moyo Suleimani kuwa hodari na mwenye moyo mkuu pasipo kufadhaika maana Bwana alikuwa pamoja naye, asingempungukia wala kumuacha katika kuijenga nyumba ya Bwana. Daudi anapomwambia Suleimani kuijenga nyumba ya Bwana anamuita kumzalia Bwana matunda, maana nyumba ingetumika kumwabudu na kumtolea Bwana sadaka. Nasi tunaalikwa kumzalia Bwana matunda mema tukiifanya kazi yake kwa bidii na uaminifu siku zote. Amina
Tunakutakia wiki njema yenye kumzalia Bwana matunda. Amina
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650