Date: 
26-01-2026
Reading: 
Isaya 42:1-9

Jumatatu asubuhi tarehe 26.01.2026

Isaya 42:1-9

[1]Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu.

[2]Hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njia kuu.

[3]Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli.

[4]Hatazimia, wala hatakata tamaa, hata atakapoweka hukumu duniani; na visiwa vitaingojea sheria yake.

[5]Mungu BWANA anena, yeye aliyeziumba mbingu, na kuzitanda; yeye aliyeitandaza nchi na mazao yake; yeye awapaye pumzi watu walio juu yake; yeye awapaye roho wao waendao ndani yake.

[6]Mimi, BWANA, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa;

[7]kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa.

[8]Mimi ni BWANA; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu.

[9]Tazama, mambo ya kwanza yamekuwa, nami nayahubiri mambo mapya; kabla hayajatokea nawapasheni habari zake.

Yesu ajidhihirisha katika utukufu wake;

Isaya analeta ujumbe wa Mtumishi aliye nuru kwa mataifa. Katika mstari wa 6, Bwana anawaita watu wake kwa haki kumwendea yeye, wakawe nuru kwa mataifa. Anawatuma kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa wafungwa gerezani na kuwatoa watu gizani. Kumbe ni agizo la Bwana tuwasaidie wenzetu kuja kwa Yesu, na tuitangaze kweli yake.

Bwana anapojidhihirisha kwa Kanisa lake, anatujia sote. Mimi na wewe tunawajibika kuwa nuru kwa wengine, wamjue na kumpokea, ili akija kulichukua Kanisa asibaki hata mmoja. Tumhubiri Kristo kila mmoja kwa nafasi yake, ili kama alivyodhihirika kwetu, adhihirike kwa wengine. Kubwa zaidi tudumu katika imani yetu, ili akirudi katika utukufu wake asituache. Amina

Jumatatu njema

Heri Buberwa Nteboya