Date: 
19-06-2025
Reading: 
1Wakorintho 2:10-16

Utatu Mtakatifu;

Alhamisi asubuhi tarehe 19.06.2025

1 Wakorintho 2:10-16

10 Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.

11 Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu.

12 Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu.

13 Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni.

14 Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.

15 Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu.

16 Maana, Ni nani aliyeifahamu nia ya Bwana, amwelimishe? Lakini sisi tunayo nia ya Kristo.

Mungu mmoja;

Baba, Mwana na Roho Mtakatifu;

Mtume Paulo anaonesha kwamba kwa kufunuliwa kwa Roho Mtakatifu, Roho huchunguza hata mafumbo ya Mungu. Paulo anahoji kwamba ni binadamu yupi aweza kujua mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Kumbe vivyo hivyo mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye, ila Roho wa Mungu. Paulo anasema Roho alishuka ili tuyajue tuliyokirimiwa na Mungu. Paulo anaendelea kukazia kwamba asiyempokea Roho wa Mungu hawezi kufunuliwa mambo ya Roho wa Mungu.

Paulo anaongelea utendaji wa Roho Mtakatifu asaidiaye waaminio kutambua mambo ya Rohoni. Naweza kusema katika somo la leo asubuhi Paulo anaongelea nafsi ya tatu ya Mungu, yaani Roho Mtakatifu kama Mungu atusaidiaye kutambua mambo ya Rohoni. Kumbe Roho huyu, ni yule yule Mungu mmoja, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Tutayatambua mambo ya Rohoni kwa msaada wa Roho Mtakatifu, Mungu mwenyewe. Amina

Alhamisi njema 

 

Heri Buberwa