Utafu Mtakatifu;
Ijumaa asubuhi tarehe 20.06.2025
Wakolosai 1:21-29
21 Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa;
22 katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili awalete ninyi mbele zake, watakatifu, wasio na mawaa wala lawama;
23 mkidumu tu katika ile imani, hali mmewekwa juu ya msingi, mkawa imara; msipogeuzwa na kuliacha tumaini la Injili mliyosikia habari zake, iliyohubiriwa katika viumbe vyote vilivyo chini ya mbingu; ambayo mimi Paulo nalikuwa mhudumu wake.
24 Sasa nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu; tena nayatimiliza katika mwili wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani, kanisa lake;
25 ambalo nimefanywa mhudumu wake, sawasawa na uwakili wa Mungu, niliopewa kwa faida yenu, nilitimize neno la Mungu;
26 siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake;
27 ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa, nao ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu
28 ambaye sisi tunamhubiri habari zake tukimwonya kila mtu, na kumfundisha kila mtu katika hekima yote, tupate kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo.
29 Nami najitaabisha kwa neno lilo hilo, nikijitahidi kwa kadiri ya kutenda kazi kwake atendaye kazi ndani yangu kwa nguvu.
Mungu mmoja;
Baba, Mwana na Roho Mtakatifu;
Asubuhi ya leo tunamsoma Mtume Paulo akiandika juu ya ukuu wa Kristo ambaye amewapatanisha watu wake na Baba. Paulo anasema kwa kifo cha Yesu wote wameletwa kwake, hivyo kuwasihi wote waaminio kusimama katika imani kwa kuiamini Injili ambayo Paulo aliihubiri. Katika ukuu huo wa Kristo, Paulo anasema anayafurahia mateso, kwa sababu ni katika njia hiyo amefanyika kuwa mhudumu wa Injili.
Paulo anaonesha ukuu wa Kristo atokaye kwa Baba, huyo ambaye alituachia Roho Mtakatifu. Huyo ndiye Paulo anasema anamhubiri bila woga akionya na kufundisha katika hekima yote ili apate kuwaleta watu wote kwa Kristo. Kwa hiyo imani katika Mungu wa Utatu ndiyo imani ya kweli, ambayo tunakumbushwa kudumu katika hiyo. Amina
Ijumaa njema
Heri Buberwa