Date: 
08-12-2025
Reading: 
Luka 21:25-28

Hii ni Advent 

Jumatatu asubuhi tarehe 08.12.2025

Luka 21:25-28

[25]

Tena, kutakuwa na ishara katika jua, na mwezi, na nyota; na katika nchi dhiki ya mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake;

[26]watu wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazamia mambo yatakayoupata ulimwengu. Kwa kuwa nguvu za mbinguni zitatikisika.

[27]Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi.

[28]Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia.

Changamkeni Mkombozi yu karibu;

Tunaendelea na majira haya ya Majilio, tunapoendelea kukumbushwa habari za ujio wa Yesu. Juma lililopita tuliona kuwa Bwana analijia Kanisa lake, na Yesu leo anaendelea kueleza juu ya kuja kwa mwana wa Adamu, ambaye ni yeye mwenyewe (Yesu). Baada ya kuwaambia mateso yatayotokea, leo Yesu anakaza juu ya mambo matatu;

1.Dalili

Katika mstari wa 26, Yesu anaongelea dalili zitakazoonyesha ujio wa Yesu ikiwemo dhiki ya mataifa, habari ambazo hata mitume walizisema na kuziandika kama vile vita, njaa, Upendo kupoa, uharibifu n.k

Ni mambo ambayo yamekuwepo, yapo. 

Yamekuwepo, yakidhihirisha kuwa ufalme wa Mungu umekuwepo, na upo, na utakuwepo. Kikubwa zaidi ni kutengeneza njia zetu, ili Bwana asituache. Maisha yetu lazima yawe ya uchaji wakati wote.

2.Tusihangaike kama wasivyoamini.

Katika somo tulilosoma, Bwana Yesu anaonyesha wenye hofu watakavyovunjika moyo kwa mambo yatakayoupata ulimwengu, kwa kuwa mbingu zitatikisika.

Hapa Bwana Yesu alikuwa akiongelea wenye Imani haba, wasioamini, au/wasiojiandaa watakavyohangaika siku Yesu akirudi. Kwa nini uwe mmojawapo wakati anayekuja ndiye mwokozi wetu? Na tunakwenda kwetu mbinguni? Yesu anasema atakuja kwa utukufu mwingi, kwa nini akuache?

Hebu tujichunguze mienendo yetu, kwamba Yesu akija, nini kitatuzuia kwenda naye? Yaani muda wote umesali na kumtumikia Mungu kwa njia mbalimbali, halafu Yesu anarudi unaanza kuwa na hofu?????

Suluhisho ni kuishi kwa Imani, ukitenda mema, bila kusahau toba na msamaha.

3.Ukombozi wetu umekaribia.

Kwa kuwa yote yameshaanza kuonekana, Yesu anatuambia tuchangamke, tuinue vichwa vyetu kwa kuwa ukombozi wetu umewadia.

Hapa Bwana Yesu anatuambia kuwa, tukiishi kwa kulifuata neno lake, dalili zote tutaziona, na Yeye tutamuona akirudi, hivyo tusiogope wala kuwa na wasiwasi, maana ukombozi wetu utakuwa umekaribia. Tunaitwa kudumu katika wokovu, ili tuuone ukombozi wetu ukikaribia.

Leo asubuhi tumesoma kuwa Yesu atakuja kwa utukufu mwingi (27). Utukufu wa Yesu hauna "ubia" na Ufalme wake hauna "ubia". "Yesu anakuja katika ufalme wake kwa utukufu mwingi. Hatuwezi kuingia kwenye ufalme wake tukiwa waovu! Tena ufalme wenye utukufu!

Umejiandaaje kuingia kwenye Ufalme wa Mungu?

 

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650

bernardina.nyamichwo@gmail.com