Date: 
17-06-2025
Reading: 
Matendo ya Mitume 2:33-36

Utatu Mtakatifu;

Jumanne asubuhi tarehe 17.06.2025

Matendo ya Mitume 2:33-36

33 Basi yeye, akiisha kupandishwa hata mkono wa kuume wa Mungu, na kupokea kwa Baba ile ahadi ya Roho Mtakatifu, amekimwaga kitu hiki mnachokiona sasa na kukisikia.

34 Maana Daudi hakupanda mbinguni; bali yeye mwenyewe anasema, Bwana alimwambia Bwana wangu, Keti upande wa mkono wangu wa kuume.

35 Hata nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako.

36 Basi nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulibisha kuwa Bwana na Kristo.

Mungu mmoja;

Baba, Mwana na Roho Mtakatifu;

Neno la asubuhi ya leo ni sehemu ya hotuba ya Petro siku ile ya Pentekoste. Petro aliwahutubia umati uliokuwapo, akitoa historia ya ukombozi wa Israeli hadi ujio wa Yesu Kristo, kufa hadi kufufuka kwake. Petro anawaambia kwamba yule waliyemkataa na kumsulibisha ndiye Mwokozi wa ulimwengu, hivyo anawaita kumwamini kwa kutubu dhambi na kubatizwa ili waokolewe.

Hotuba ya Petro inaakisi Utatu Mtakatifu. Petro anamtaja Mungu aliyemtuma mwana wake ulimwenguni (33), anamtaja Yesu aliyesulibishwa (36) na Roho Mtakatifu aliyewashukia Mitume (33). Kumbe Petro anamhubiri Mungu mmoja katika Utatu Mtakatifu, akiwaita watu kuokolewa. Tusiyumbe katika imani yetu kwa Mungu mmoja aliye katika Utatu Mtakatifu, tuko sehemu sahihi na salama. Amina

Jumanne njema

Heri Buberwa Nteboya