Date: 
24-06-2025
Reading: 
1 Timotheo 6:11-16

Jumanne asubuhi tarehe 24.06.2025

1 Timotheo 6:11-16

11 Bali wewe, mtu wa Mungu, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa, imani, upendo, saburi, upole.

12 Piga vita vile vizuri vya imani; shika uzima ule wa milele ulioitiwa, ukaungama maungamo mazuri mbele ya mashahidi wengi.

13 Nakuagiza mbele za Mungu anayevihifadhi hai vitu vyote, na mbele za Kristo Yesu, aliyeyaungama maungamo mazuri yale mbele ya Pontio Pilato,

14 kwamba uilinde amri hii pasipo mawaa, pasipo lawama, hata kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo;

15 ambako yeye kwa majira yake atakudhihirisha, yeye aliyehimidiwa, Mwenye uweza peke yake, Mfalme wa wafalme, Bwana wa mabwana;

16 ambaye yeye peke yake hapatikani na mauti, amekaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa; wala hakuna mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye hata milele. Amina.

Tuyashike sana maungamo yetu;

Mistari inayotangulia somo la asubuhi la leo (3 hadi 10) inaelekeza kuyaepuka mafundisho ya uongo. Sasa kuanzia mstari wa 11 ambao ndipo somo linaanzia ni wito wa kuachana na hayo mafundisho ya uongo na kuifuata haki, utauwa, imani, na kuishika njia ya uzima wa milele. Somo linaonesha kuwa Kristo aliyaungama maungamo mazuri mbele ya Pilato, yaani hakuikana imani japokuwa aliona mateso yakimjia. 

Agizo tunalopewa asubuhi hii ni kuhifadhi mafundisho ya neno la Mungu mioyoni mwetu kwa mfano wa Yesu Kristo ambaye hakuikana imani mbele ya Pilato. Tunaweza kupitia changamoto mbalimbali katika maisha yetu, lakini changamoto hizo zisitutoe katika njia sahihi, ambayo ni Kristo Yesu. Tuilinde amri ya Kristo (14) yaani kuyashika maungamo yetu ili tutende kwa usahihi katika yeye aliyetuita. Amina

Jumanne njema

Heri Buberwa