Date: 
27-06-2025
Reading: 
Waebrania 3:1-6

Ijumaa asubuhi tarehe 27.06.2025

Waebrania 3:1-6

1 Kwa hiyo, ndugu watakatifu, wenye kuushiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini sana Mtume na Kuhani Mkuu wa maungamo yetu, Yesu,

2 aliyekuwa mwaminifu kwake yeye aliyemweka, kama Musa naye alivyokuwa, katika nyumba yote ya Mungu.

3 Kwa maana huyo amehesabiwa kuwa amestahili utukufu zaidi kuliko Musa, kama vile yeye aitengenezaye nyumba alivyo na heshima zaidi ya hiyo nyumba.

4 Maana kila nyumba imetengenezwa na mtu; ila yeye aliyevitengeneza vitu vyote ni Mungu.

5 Na Musa kweli alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu kama mtumishi, awe ushuhuda wa mambo yatakayonenwa baadaye;

6 bali Kristo, kama mwana, juu ya nyumba ya Mungu; ambaye nyumba yake ni sisi, kama tukishikamana sana na ujasiri wetu na fahari ya taraja letu mpaka mwisho.

Tuyashike sana maungamo yetu;

Mwandishi wa waraka kwa Waebrania anaonesha tofauti kati ya Musa na Yesu Kristo, kwamba Musa alikuwa mtumishi lakini Yesu ni mwana wa Mungu, Mwokozi. Musa aliifanya kazi yake kwa uaminifu wote, lakini Kristo amestahili Utukufu kuliko Musa kama vile aijengaye nyumba alivyo na heshima kuliko nyumba yenyewe.

Inaonekana waraka huu uliandikwa kwa baadhi ya watu walioendelea kuishika sheria ya Musa, kwamba pamoja na kufufuka kwa Yesu bado wao waliiweka sheria mbele. Kumbe Yesu Kristo ndiye alikuwa utimilifu wa hiyo sheria. Maungamo yetu yanatuongoza kwamba Yesu ni Mwokozi wa ulimwengu. Tumwamini yeye peke yake daima. Amina

Ijumaa njema

 

Heri Buberwa Nteboya