Jumanne asubuhi tarehe 27.01.2026
Kutoka 3:1-6
1 Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu.
2 Malaika wa Bwana akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea.
3 Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei.
4 Bwana alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa.
5 Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu.
6 Tena akasema, Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu.
Yesu ajidhihirisha katika utukufu wake;
Musa akiwa anachunga anatokewa na malaika wa Bwana, katika mwali wa moto Musa anaona kijiti ambacho hakiteketei. Musa anageuka kutazama yanayojiri, ndipo Bwana anamuita akimwambia avue viatu vyake maana alipo ni nchi takatifu. Mungu anajitambulisha kwa Musa kama baba wa babu zake, wakati huo Musa akiwa ameficha uso wake maana aliogopa kumwangalia Mungu.
Ukiendelea kusoma unaona kwamba ndiyo wakati Mungu alikuwa anamuita Musa kwa ajili ya kwenda kuwatoa Israeli Misri. Hivyo anatumwa kwa Farao akawatoe wana wa Israeli, tayari kuwaongoza kuelekea nchi ya ahadi. Kwa hiyo safari ya wana wa Israeli kuelekea Kanaani ilianza kwa Mungu kujifunua kwa Musa. Mungu aliendelea kujifunua kwa watu wake, sasa kwa njia ya Yesu Kristo aliye Mwokozi wetu. Mwamini sasa uokolewe. Amina
Jumanne njema
Heri Buberwa
